UCHAMBUZI WA MAUDHUI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Kuna maudhui kadhaa yanayojitokeza kwenye tamthilia ya Kigogo iliyoandikwa naye Pauline Kea. Haya ndio baadhi ya maudhui hayo:

1) UONGOZI MBAYA

Viongozi huangaisha wanyonge, Ashua anasema,

“…na kuhangaishwa na wenye nguvu ndio

hewa tunayopumua huko.” (uk 2)

Wachochole hutumikizwa na viongozi, Kombe, Boza na Sudi wanafanya kazi ya kuchonga vinyago vya mashujaa kwa ajili ya sherehe za uhuru.

Viongozi hawajawajibika, kazi yao ni kukusanya tu kodi.Ni jukumu la viongozi kuhakikisha kuwa soko ni safi lakini hawajawajibika kulisafisha. Licha ya wananchi kutoa kodi,soko ni chafu.(uk 2)

Viongozi kutangaza kipindi kirefu cha kusheherekea uhuru ni ishara ya uongozi mbaya.Mashujaa wanaenziwa kwa kipindi kirefu ilhali mambo ya kimsingi hayajazingatiwa.Wanasagamoyo wana matakwa mengi kuliko kipindi kirefu cha kusherehekea uhuru.

Majoka anafadhili mradi usio na msingi wa kuchonga vinyago huku watu wakiwa na njaa na wao ndio watalipia mradi huo.

Viongozi hushawishi wananchi kwa ahadi ili wawaunge mkono.Sudi anashawishiwa na Kenga kuchonga kinyago ili apate malipo mazuri;kuwa mradi huo utabadilisha maisha yake na jina lake lishamiri. Pia atapata tuzo nyingi na likizo ya mwezi mzima ughaibuni na familia yake (uk 11)

Aidha viongozi hutumia zawadi kufumba wananchi kuwa wanawajali na kujali hali zao.Kenga anawaletea Sudi, Boza na kombe keki ya uhuru.

Kulingana na Sudi, hayo ni makombo na keki kubwa imeliwa kwingineko.

Viongozi hawalindi usalama wa wananchi,wananchi wanaishi kwa hofu. Ashua anahofia usalama wao kuwa huenda wakashambuliwa.(uk 15)

Migomo inayotokea Sagamoyo na maandamani ni kwa sababu ya uongozi mbaya.Wauguzi wanagoma na pia walimu wakidai haki zao.Wafanyakazi wananyanyaswa.

Majoka hajali maslahi ya wanasagamoyo.Anafunga soko ambalo wananchi wanategemea na kupandisha bei ya chakula.Uchumi Sagamoyo unasorota kutokana na soko kufungwa, watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa zao.

Majoka anafungulia biashara ya ukataji miti bila kujali hali ya anga Sagamoyo,hasara ni kwa maskinii, viongozi wamejichimbia visima.Mito na maziwa yanakauka na mvua isiponyesha, hata maji ya kunywa yatatoka ng`ambo.

Majoka hajali kuhusu kifo cha Ngurumo licha ya kuwa mfuasi wake.Anaagiza Ngurumo azikwe kabla ya jua kutua (uk 69)

Viongozi hupanga njama ilikuangamiza wapinzani wao;

a) Majoka na Kenga wanapanga njama ya kumtia Ashua ndani.Wanapanga aitwe ofisini mwa Majoka kisha Husda aitwe ili wafumaniane.Ashua anazingiziwa kuzua sogo katika ofisi ya serikali na kutiwa ndani.Husda anafunguliwa baada ya nusu saa.

b) Kifo cha Jabali kilipangwa.Jabali alikuwa mpinzani wa Majoka mwenye wafuasi wengi. Akapangiwa ajali barabarani kisha wafuasi wake wakazimwa na kumfuata jongomeo,chama chake cha mwenge kilimfuata ahera.

c) Tunu anapanga kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali ya Jabali. Majoka anapopata habari hizi,anapanga kuzima uchunguzi huo.

d) Kenga na Majoka wanapanga kuondoa chatu mmoja. Chatu hapa wanarejelea Sudi au Tunu kwa kuwa ndio wanaoongoza mapinduzi. Wanahofia kutolewa uongozini na ili kuzuia hali hii, wanapanga kumwondoa mmoja wao.

“…chatu mmoja atolewe kafara ili watu wajue usalama upo,wakereketwa waachwe katika hali ya taharuki”

e) Majoka anapanga njama Tunu auliwe,anaumizwa mfupa wa muundi nia yake ikiwa ni kumkomesha asimpinge. Majoka anatumia polisi wake kutekeleza ukatili huo.

Katika hotuba ya Tunu anayowahutubia waandamanaji,Sagamoyo kuna uongozi mbaya.Anasema kuwa;

  • pesa za kusafisha soko zimefujwa,
  • soko linafungwa badala ya kusafishwa,
  • haki za wauzaji zimekiukwa.

Viongozi hawasikilizi matakwa ya wananchi.Majoka hana wakati wa kuwasikiliza waandamanaji.Hataki kujua chanzo cha maandamano wala suluhu lake.

Majoka anadhibiti vyombo vya habari Sagamoyo, habari zinazopeperushwa katika runinga ya Mzalendo na picha za watu wengi sokoni wakiongozwa na Tunu zinamfanya Majoka kufunga runinga hiyo ya mzalendo.

Viongozi hutumia vitisho.Majoka anatishia Chopi kumwaga unga wake kwa vile polisi hawakuwatawanya waandamanaji,wanasagamoyo wanatishiwa kuhama Sagamoyo kwa juwa sio kwao,wanarushiwa vijikaratasi. (uk 52)

Majoka anatumia askari kutawanya raia badala ya kulinda uhuru wao.

Viongozi ni waongo.Majoka anatumia uongo ili kumteka Tunu.Anamhaidi jambo la kifahari, kumwoza Ngao Junior akirudi kutoka ng`ambo.

viongozi hutendea wananchi ukatili,watu wanaotiwa jela huchapwa na haki zao hukiukwa.Ashua ana majeraha kutokana na kichapo.

Viongozi hupanga uvamizi, Sudi anavamiwa (uk 54)

Viongozi wamekiuka sheria.Mamapima anadai kuwa anauza pombe haramu kwa kibali kutoka serikali ya Majoka.Ni hatia kuuza pombe haramu lakini viongozi huvunja sheria na kuwapa wauzaji kibali. (uk 61)

Sagamoyo hata viongozi hawafuati katiba.

“…huku ni Sagamoyo, serikali na katiba ni mambo mawili tofauti.” (uk 61)

Uongozi wa Majoka una ubaguzi, unafaudi wachache tu, wanaomuunga mkono.Asiya bibiye Boza anapata mradi wa kuoka keki mwa vile anauunga uongozi wa Majoka Mkono.

Viongozi hujulimbikizia mali. Kuna hoteli ya kifahari Sagamoyo,Majoka and Majoka modern resort.

Viongozi ni wanafiki.Majoka amepanga kuficha maovu yake mbele ya wageni.Ukumbi unapambwa na kurembeshwa huku kukiwa na maovu mengi Sagamoyo.Kuna mauaji, unyakuzi, njaa,maziara yamejaa Sagamoyo.

2) UZALENDO

Wananchi wa Sagamoyo ni wazalendo, wanalipa kodi ili kuleta maendeleo licha ya kulaghaiwa.

Katika enzi za ukoloni, mashujaa walijitolea mhanga wakahatarisha maisha yao na hata kufa ili wavune matunda baada ya uhuru. (uk 4)

Wimbo unaoimbwa katika rununu ni wa kizalendo kuonyesha kuwa wanasagamoyo wanalipenda jimbo lao, sagamoyo.(uk 5)

Sudi anaelewa kuwa uongozi wa Majoka haufai.Anawaeleza Boza na Kombe umuhimu wa kuandika historia ya Sagamoyo upya.Kinyago anachokichonga Sudi ni cha shujaa halisi wa Sagamoyo,anaelewa kuwa Tunu ndiye anapaswa kuwa kiongozi halisi.

Tuni ni mzalendo katika taifa lake. Anasema kuwa jukumu lake ni kulinda uhai, haki na uhuru.Amajitolea kwa vyovyote vile kutetea haki Sagamoyo.Wamekula kiapo kutetea haki Sagamoyo hata kama ni kwa pumzi zao za mwisho baada ya mafanikio. (iuk18).Akiwa mwanafunzi katika chuo kikuu walipambana kama viongozi wa chama cha wanafunzi chuoni hadi kuleta mafanikio.

Tunu ni mzalendo Sagamoyo, anawahutubiawananchi na kuwaarifu hali ilivyo Sagamoyo.Pesa za kusafisha soko zimefujwa,soko limefungwa badala ya kusafishwa na haki za wauzaji kukiukwa.Wamejitolea kutolegeza msimamo wao hadi soko lifunguliwe.

Tunu anamkabili Majoka kwa uovu wake.Anamwambia wazi kuwa atalipa kila tone la damu alilomwaga Sagamoyo,yeye na watu wake. (uk 43)

Tunu anatetea maslahi ya wanyonge, anamwambia Majoka kuwa Wanasagamoyo wana haki ya kuishi,anamwambia ugatuzi si unyakuzi na kumkashifu kwa kubomoa vioski katika soko la Chapakazi.(uk 45)

Tunu anamkashifu mamapima kwa kuuza pombe haramu kwa vile ni kinyume cha sheria.Anatetea katiba ya nchi inayofafanua sheria zinazohusiana na uuzaji na unywaji wa pombe.

Tunu anajitolea kuwatumikia wanasagamoyo.Yeye ni mtu wa vitendo na wala si vishindo.Anaita mkutano ili soko lifunguliwe na kuapa kutoondoka hadi soko litakapofunguliwa.Tunu amejitolea kuikomboa Sagamoyo ili kuleta mabadiliko,anakiri kuwa mambo hayatapoa, kumewaka moto na kutateketea.(uk 55)

3) NAFASI YA MWANAMKE

Sudi anapochonga kinyago cha shujaa mwanamke,Kenga anamwambia Sagamoyo haijawahi kuwa na shujaa mwanamke.Katika historia ya Sagamoyo wanawake wametengwa katika uongozi.(uk 10).

Kenga anasema kinyago hicho hakitanunuliwa na afadhali achonge kinyago cha Ngao.

Wanawake wamesawiriwa kuwa hawara,Sudi anapokataa kuchonga jinyago,Kenga anamwambia kuwa amelishwa kiapo na hawara wake.(uk12)

Wanawake hutumiwa kama pambo katika jamii ya Sagamoyo.Majoka anamwambia Ashua kuwa,urembo wake hauna mfanowe.

“…nikufanishe na nini? urembo wako hauna mfanowe Ashua”(uk 20)

Majoka anamshauri Ashua atumie urembo wake kwa kuwa ni wa muda.(uk 25)

Husda anakiri kuwa mwanamke ni pambo mbele ya mwanamme.(uk67)

Wanawame wamesawiriwa kuwa wenye maringo.Majoka anadai kuwa Ashua alikataa kazi ya ualimu kwa sababu ya maringo.(uk25)

Wanawake wamadharauliwa.Majoka anawadharau Ashua na Husda kwa kusema wanawake ni wanawake tu,si kitu mbele yake.(uk 26)

Adui wa mwanamke ni mwanamke.Husda anamwita Ashua mdaku, kimada wa kuwinda wanaume wa watu.Hali halisi ni kuwa,Ashua hana nia hii.

Majoka anamweleza Sudi kuwa mkewe Ashua hajui maana ya ndoa.Anasema kazi yake ni kuzururasurura .wanawake hulaumiwa.

Mwanamke amedharauliwa, mvamizi anamkanya Tunu aache kunyemelea wanaume wa watu.

Ngurumo anamdharau Tunu kwa kuwa mwanamke.Anaposema soko lifunguliwe, Ngurumo anamdharau na kumuuliza yeye ni nani Sagamoyo,wanawake hawatambuliwi.

Mwanamke katika jamii ya Sagamoyo ni kuolewa na kumtumikia mwanamme.Wimbo wa Ngurumo kwa Tunu unamshauri aolewe, kwa kuwa ana elimu asije akazeekea nyumbani kwao.

Wanawake wamechukuliwa kuwa dhaifu kwamba hawawezi kuongoza.Majoka anasema hawezi kuaibishwa na mwanamke.(uk 90)

Hata hivyo, wanawake ni wasomi,Ashua ana shahada ya ualimu.

Wanawake wamajipigania kujikomboa.Tunu anakataa kuozwa kwa Ngao Junior na kujitetea kuwa anaweza kusubiri aolewe na mume ampendaye.(uk42)

Mamake Tunu anajifunga kibwebwe baada ya kifo cha babake ili Majoka agharamie masomo ya Tunu.

Wanawake ni wanamapinduzi na viongozi bora.Tunu anaongoza mapinduzi ili kuleta haki Sagamoyo.

4) MIGOMO/MAANDAMANO

Wauguzi Sagamoyo wanaandamana.

Walimu Sagamoyo wanagoma wakiwa likizoni.

Kiwandani Majoka and Majoka company anapofanya kazi siti,watu wanagoma.Vijana watano wanauliwa..

Wachuuzi sokoni wanaandamana,wengine wanaumizwa.Wanaandamana kwa sababu ya soko kufungwa.Wanaume Sagamoyo ni kukimbizana na waandamanaji.

Waandamanaji huandamana kila siku, kuna picha za waandamanaji gazetini kila siku.

Habari gazetini zinaonyesha kuwa Tunu ameongoza maandamano na anaandamana na wanaojiita wanaharakati.(uk 32)

Tunu anawahutubia wanahabari na kusema kuwa pesa za kusafisha soko zimefujwa, soko kufungwa badala ya kusafishwa. (uk 33)

Kenga anamshauri Majoka ayapuuze maandamabo yanayoendelea.(uk 34)

Kuna habari kwenye mtandao wa mijamii kuhusu maandamano.Watu wengi wanaandamana sokoni wakiongozwa na Sudi.Maandamano yanazidi kuharibia sherehe ya uhuru.

5) MATUMIZI MABAYA YA VYOMBO VYA DORA

Majoka anatunia polisi kuwatawanya waandamanaji na kuwaumiza wapinzani wake,Tunu anaumizwa mguu.

Runinga ya mzalendo haina maisha Sagamoyo kwa sababu ya kupeperusha habari za maandamano. Majoka anaamua kufunga vituo vya habari na kibakie tu kituo kimoja.

Kenga anamshauri Majoka waichukulie hatua runinga ya mzalendo kwa kuwa haipendi yeye.

Majoka anatumia vyombo vya habari kuimba nyimbo za kizalendo ili kumsifu yeye.

Vyombo vya habari hueneza propaganda,kuna habari katika vyombo vya habari kuwa Tunu hawezi kupigania haki za Wanasagamoyo kwa kuwa amelemazwa mguu.

6)ASASI YA NDOA

a)NDOA KATI NYA ASHUA NA SUDI

Ni ndoa yenye mapenzi yanayoegemea upande mmoja.Sudi anampenda Ashua kwa dhati,anajitahidi kwa udi na uvumba ili kumkidhi Ashua.Kila kitu anachokipata humletea.

Sudi ni mwaminifu katika ndoa yake,hajamwenda Ashua kinyume hata Ashua anapotiwa ndani na Majoka.

Aidha, ndoa hii imejengwa katika misingi ya kutoaminiana.Ashua anamshuku mumewe kuwa ana mipango ya kimapenzi na Tunu.

Ashua amechoshwa na Sudi na anaswema kuwa ni afadhali alipo jelani. Anadai kuwa, mawazo ya Sudi,hisia zake, nafsi yake ma kila kitu chake kimesombwa na Tunu.

Ashua ametawalwa na tamaa ya mali na kumwambia Sudi kuwa amechoka kupendwa kimaskini, anabadilika akiwa ndani kwa Majoka, awali alimpenda mumewe kwa dhati lakini baadaye anaomba talaka.Anafurikwa na tamaa na ubinafsi.

b) NDOA KATI YA MAJOKA NA HUSDA

Ni ndoa ambayo imejaa lawama,Majoka anamlaumu Husda kuwa hampendi bali aliolewa na mali yake.( uk 75)

Hakuna mapenzi ya dhati katika ndoa hii.Majoka hampendi Husda. Alimoa ili kutimiza wajibu wake katika jamii na kama kiongozi,alipaswa kuoa.Alilia usiku huo baada ya kumwoa Husda lakini moyo na nafsi yake viko kwa Ashua.(uk75)

Majoka anampenda Ashua zaidi ya kumpenda hata anaweza kumfia. Anapanga njama ili kumpata. Majoka anakiri kuwa Ashua anamuua moyoni kwa penzi. Anamkondesha na kumkosesha raha kwa kumkataa.Ashua kumkimbia Majoka alimwachia Majoka aibu na penzi lake kwa Ashua linamsongoa.(uk 76).

Asasi ya ndoa imo hatarini kwa kutawaliwa ma tamaa ya mali.Baadhi ya wanaume huoa ili kutimiza matakwa yao na wanawake huolewa kwa sababu ya tamaa ya mali na ubinafsi.

Wanaume wanapaswa kujidadisi na wakae na wake zao kwa heshima.Wanawake nao wanapaswa kujirudi vinginevyo asasi ya ndoa imo hatarini.(uk 77)

Uaminifu na mapenzi ya kweli ni kigezo muhimu ili ndoa idumu.

7) ULEVI NA ATHARI ZAKE

Mangweni kwa mamapima shughuli za ulevi zimeshika kani.

Ngurumo ni mlevi kupindukia, anajulikana Sagamoyo kwa uraibu wake wa vileo.Anajunywa pombe zaidi ili kusherehekea sherehe za uhuru.

Vijana ni walevi kwa mamapima hadi wanasimama kwa taabu.

Ulevi umepotosha baadhi ya vijana,Ngurumo alisoma darasa moja na Tunu lakini ni mlevi kupindukia, hajitambui.

Kwa mamapima kila mtu hupewa vileo kwa raha zake.

Ulevi umemfumba Ngurumo hadi haoni athari za soko kufungwa,yeye anadai kuwa yuko sawa na hataki soko lifunguliwe.(uk60)

Mamapima hatambui hatari za ulevi,anaona kulewa ni raha,anawaambia Tunu na Sudi wajipe raha kwa kulewa.

Mtu mmoja ni hoi kutokana na ulevi,anaanguka chini na kuanza kugaragara.

Tunu anasema kuwa juzi waliwazika watu kutokana na pombe na wengine kugeuka vipofu kwa sababu ya pombe.

8) VIFO/MAUAJI

Vijana watano wanauliwa watu wanapoandamana katika kampuni ya Majoka.

Watu huuliwa Sagamoyo.

“Natumai hakuna aliyeuliwa,sitaki kujipaka matope tena” (uk 31)

Kifo cha Jabali kilipangwa katika ajali kwa kuwa mpinzani wa majoka hata chama chake cha Mwenge kikamfuata ahera.

Tunu anamwambia Majoka kuwa yeye na wenzake ni wauaji.(uk43)

Viongozi humwaga damu Sagamoyo.Tunu anamwambia Majoka kuwa atalipa kila tone la damu lililomwagwa Sagamoyo.

Babake Tinu anakufa katika Majoka and Majoka company.Marara na watu wake walimtemdea ukatili.

Hashima anasema damu nyingi imemwagika Sagamoyo hadi ardhi imeingia najisi.

Mashujaa wengine walienda jongomeo kwa kuleta uhuru Sagamoyo.

Ngurumo ananyongwa na chatu akitoka Mangweni.

Majoka anapanga kutekeleza mauaji kwa kumwondoa chatu mmoja ili pawe na usalama Sagamoyo.Kuomdoa chatu ni kuua Sudi au Tunu.

Kifo cha Ngao junior kinatokea, anapatikana katika uwanja wa ndege akiwa na sumu ya nyoka.

Majoka anasema kuwa ziwa kubwa limefurika damu furifuri kumaanisha vifo vya watu wengi vimetokea Sagamoyo.Watu wanalilia damu ya Majoka, wanataka kumuua.(uk 79)

9) UFISADI

Serikali ya Majoka ina ufisadi, inampa mamapima kibali cha kuuza pombe haramu.

Mamapima ni fisadi,anawapunja walevi.

Majoka anatumia pesa za umma visivyo kugharamia njama ili kuzima uchunguzi wa Tunu kuhusu ajali ya Jabali.

Viongozi Sagamoyo ni fisadi,wanaitisha kitu kidogo kutoka kwa wananchi.Wakati mwingine viongozi hudai kitu kikubwa au kitu chote.(uk 3)

Viongozi hutumia mali ya umma visivyo kufadhili miradi isiyo muhimu,kufadhili mradi wa muchonga vinyago ni kufisidi wananchi maana watalipia mradi huo.

Majoka anafisidi wananchi kwa kufunga soko ili ajenge hoteli ya kifahari.Soko ni chafu ilihali wananchi wanalipa kodi ya kusafisha soko.Majoka anadai kuwa ana mradi muhimu wa mushughulikia kuliko kusafisha soko.

Majoka ni fisadi, alikuwa na mpango wa kumpa Ashua kazi ya ualimu katika Majoka and Majoka academy kwa njia isiyo halali.

10) USALITI

Majoka anawasaliti wanasagamoyo,watu wote wanamhukumu kwa kuwasaliti.

Majoka anatumia polisi kuwatisha wanasagamoyo badala ya kulinda usalama wao akiwa kiongozi wao.

Kingi anamsaliti Majoka wakati wa mwisho,anampinga amri yake kuwapiga watu risasi, siku zote alimtii Majoka.

Majoka anawasaliti wanasagamoyo kwa kuwafungia soko,anapaswa kulisafisha badala ya kulifunga.

Majoka anawasaliti wanasagamoyo kwa kupanga mauaji badala ya kulinda na kutetea haki zao.

Ashua anamsaliti Sudi kwa kuomba talaka licha ya kuwa sudi anampenda kwa dhati.

Boza na Kombe wanawasaliti wanamapinduzoi kwa kuunga mkono uongozi mbaya wa Majoka.

Majoka anamsaliti Husda kwa kukiri kuwa hampendi licha ya kuwa mkewe.

11) UTABAKA

Jamii ya Sagamoyo imegawika katika matabaka mawili;tabaka la watawala na tabaka la watawalwa.Watawala wanaishi maisha ya kifahari huku watawalwa wanaishi maisha ya uchochole.

a)watawala/walalahai

Viongozi wana madaktari wao wa kuwahudumia,Majoka anapozirai,daktari wake anaitwa.

Watawala wana shule za kifahari, Majoka and Majoka academy ni shule ya kifahari.

Watoto wa viongozi huishi ng`ambo palipo na maisha bora.Ngao Junior yuko ng`ambo.

Watawala wanaishi maisha ya starehe,

Mzee Kenga ana gari la kifahari na walinzi,

Majoka anasema apikiwe kuku kwachapati

Majoka ana hoteli la kifahari

Watawala wamejichimbia visima,Majoka anafungulia biashara ya ukataji miti huku wanasagamoyo wakiteseka kwa kiangazi.

Ofisini mwa Majoka anakalia kiti cha kifahari,kando yake kumepangwa medhali kadhaa,anaishi maisha ya kifahari.

b)Watawalwa/wachochole

Soko la Chapakazi ni la wachochole.

Wachochole wana njaa,watoto wa Sudi wanalia njaa, Sudi anakula embe bovu.

Maskini wanateseka, mvua isiponyesha hata maji ya kunywa wayatoa ng`ambo.

Wauguzi wanagoma kwa sababu ya mishahara duni huku viongozi wakiwa na madaktari wa kuwahudumia.

12) UNYANYASAJI

Wanasagamoyo wananyanyaswa.Kilicho chao kinachukuliwa na wanatishwa.

Wananchi wanatumikizwa, Sudi wanaambiwa wachonge vinyago ili kufaidi viongozi.

Wanasagamoyo wananyanyaswa,keki ya uhuru inaliwa kwingineko nawanaletewa makombo.

Wananchi wanafungiwa soko ambalo ni tegemeo lao.Hawana mahali pengine pa kuuzia bidhaa zao.

Sagamoyo watu wananyanyaswa kwa kulazimishwa kulipa kitu kidogo wakati mwingine kitu kikubwa au kitu chote.

Ashua ananyanyaswa kwa kutiwa ndani bila kosa.

13) TAMAA

Majoka ana tamaa ya uongozi,hataki kuondoka mamlakani.Anafanya kila awezalo kuondoa wapinzani wake.

Anataka kumtambulisha Ngao Junior rasmi kuwa mrithi wake kwenye siasa.

Majoka anadai kuwa hata asipopigigwa kuta moja atashinda.Ana tamaa ya uongozi.

Majoka ana tamaa ya mali,ananyakua uwanja wa soko ili kujenga hoteli ya kifahari.

Majoka anawafisidi wananchi ili kujilimbikizia mali kwa sababu nya tamaa

Mamapima ana tamaa ya mali,anawapunja walevi.

Husda ana tamaa ya mali, anaolewa na Majoka kwa sababu ya mali yake.

Tamaa inamtawala Ashua hadi anaomba talaka.Anadai amachoka kupendwa kimaskini kwa kuongozwa na tamaa ya mali.

14) UCHAFUZI WA MAZINGIRA

Kuna maji chafu ambayo yametabakaa mitaroni Sagamoyo.Povu jeupe limechacha

Soko la Sagamoyo limegeuka uwanja wa kumwaga jemikali na taka.

Uchafuzi wa mazingira unaatharisha maisha ya wanasagamoyo.Sudi anakiri kuwa nusra wafe kwa sababu ya mazingira chafu.

“…Mungu anatupenda, vinginevyo tusingekuwa hai.”

Sagamoyo hakukaliki kwa sababu ya uvundo kila mahali.


NEXT: MBINU MBINU ZA UANDISHI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO


PREVIOUS: WAHUSIKA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO


dhamira ya mwandishi katika kigogokigogo maudhuikigogo noteskigogo riwayakigogo setbook video downloadkigogo summarykigogo summary noteskigogo tamthiliakigogo tamthilia pdfkigogo videomaswali ya kigogomaswali ya tamthilia ya kigogomaudhui katika kigogo pdfmaudhui ya uzalendo katika kigogomwongozo wa kigogotamthilia ya kigogo videouchambuzi wa riwaya ya kigogowahusika wa tamthilia ya kigogo