MBINU ZA UANDISHI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Mwandishi Pauline Kea, ametumia mbinu tofauti za uandishi katika tamthilia ya Kigogo. Zifuatazo ndizo mbinu zilizotumika:

KINAYA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Habari zinazotolewa na mjumbe katika rununu ni za kinaya, kuwa wanasagamoyo wasirudishe maendeleo nyuma bali wafurahie ufanisi ambao umepatikana katika kipindi cha miaka tisini baada ya uhuru.

Ujumbe huu ni kinaya kwa vile Sagamoyo hakuna maendeleo wala ufanisi.Watu wana njaa na wanakosa mambo ya kimsingi kama vile maji, elimu na matakwa mengine mengi.

Boza anadai kuwa kulipa kodi ni kujenga nchi na kujitegemea. Kauli hii ni kinaya kwa vile kodi wanayolipa wanasagamoyo haitumiki kujenga nchi kwa vyovyote vile.

Sudi anasema kuwa katika kipindi cha mwezi mzima wa uhuru wale mali walizochuna kwa miaka sitini. Ni kinaya kwa kuwa hakuna walichovuna, viongozi hujilimbikizia mali.

Boza anamwambia Sudi kuwa wanatia doa kwa kila jambo nzuri.Ni kinaya kwa vile hakuna mambo mazuri ambayo Majoka amefanya Sagamoyo.(uk5)

Wanasagamoyo kusheherekea miaka sitini ya uhuru ni kinaya kwani hakuna cha muhimu kusheherekewa, hakuna maendeleo Sagamoyo.

Boza anadai kuwa kinyago chake chapendeza na kufanana na shujaa Marara Bin Ngao, ni kinaya kwani kinyago hicho hakifanani na shujaa huyo.

Mzee Majoka kudai kuwa anamheshimu sudi ni kinaya.Majoka hana heshima kwa raia wake, nia yake ni kutaka Sudi amchongee kinyago.(uk13)

Kenga kumwambia Sudi kuwa ipo siku atamtafuta mzee Majoka ni kinaya kwani Sudi hana haja naye.

Majoka kudai kuwa takataka za soko zitaaribu sifa nzuri za jimbo la Sagamoyo ni kinaya kwa vile hakuna sifa nzuri Sagamoyo.Viongozi wanaendeleza maovu na hata kupanga mauaji.

Kauli ya Husda kuwa Ashua ni kimada wa Majoka ni kinaya kwa vile Ashua hana nia yoyote na Majoka.Amefika kwake kuomba msaada.

Ni kinaya kwa polisi Sagamoyo kutawanya waandamanaji.Polisi wanapaswa kulinda na kutetea haki za wananchi.

Majoka kusema kuwa Sagamoyo wanajiweza ni kinaya.Watu wana matakwa mengi, ni maskini, wana njaa na hata kupata ufadhili kitoka nje kwa miradi isiyo muhimu.

Ni kinaya Kenga anapomwambia Majoka aache moyo wa huruma,kwa sababu Majoka hana hata chembe cha huruma.Anapanga mauaji na kunyanyasa raia.

Majoka anaposema kuwa juhudi za Tunu kuandaa migomo hazitamfikisha mahali ni kinaya kwa vile Tunu wanafanikiwa katika maandamano yao na hata kuungwa mkono na wengi.

Ni kinaya kwa Ashua kumwambia Sudi kuwa ni kosa lake kutiwa ndani.Kosa ni la Majoka na njama yake ya kutaka kuchongewa kinyago.

Ashua anasema kuwa katika jela kuna amani na amechoshwa na Sudi.Ni kinaya kwani Ashua anapata maumivu akiwa jelani.

Uvumi unaoenea kuwa Sudi na Ashua ndio wanaowinda roho ya Tunu ni kinaya kwani wote hawa ni wanamapinduzi wanaopigania haki Sagamoyo.

Madai ya Ngurumo ni kinaya kuwa tangu soko kufungwa Sagamoyo ni pazuri mno.Eti mauzo ni maradufu ilihali watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa zao, kifungwa kwa soko kunawaangaisha raia hata zaidi.

Ngurumo kusema kuwa pombe ni starehe ni kinaya kwani watu wanaangamia kutokana na pombe, wengine kuwa vipofu.

Watu wengi wanatarajiwa kufika katika uwanja wa ikulu ya Majoka kusherehekea uhuru siku ya sherehe lakini ni kinaya kwa kuwa ni watu kumi tu ambao wanafika.

JAZANDA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Kinyago cha shujaa anachochonga Sudi kwamba shujaa huyo nimkubwa kuliko jina lake na urembo wa shujaa huyo ni bora zaidi.Shujaa anayerejelewa hapa ni Tunu,yale ambayo anatendea Sagamoyo ni makuu kuliko jina lake, kutetea haki za wanyonge.(uk10)

Husda anamwambia Ashua kuwa hawezi kumtoa bonge kinywani hivi hivi.Bonge ni Majoka bwanake Husda kuwa Ashua hawezi kumnyanganya bwana.

Husda kumwita Majoka pwagu, pwagu ni mwizi na Majoka amewaibia wanasagamoyo;ananyakua ardhi, anaiba kodi na kuwalaghai wanasagamoyo.(uk27)

Husda anamwambia Ashua kuwa ameshindwa kufuga kuku na kanga hatamweza.Kuku ni mumewe Sudi, na Kanga ni Majoka, kwamba Ashua ameshindwa kumtunza Sudi na Majoka hampati.(uk28)

Tunu kuwekewa vidhibitimwendo ni kukomeshwa au kuwekewa vikwazo ili afe moyo kutetea haki za wanasagamoyo.

Majoka anasema kuwa hatatumia bomu kuulia mbu.Anamrejelea Tunu kuwa mbu kunaanisha hatatumia nguvu nyingi kumwangamiza.(uk35)

Majoka anasema ili kuongoza Sagamoyo ni lazima uwe na ngozi ngumu, kumaanisha ni lazima uwe mkali na mwenye nguvu.

Jukwaa kupakwa rangi kwa ajili ya sherehe ya uhuru ni kufunika uozo ulio Sagamoyo.

Majoka anaposema salamu zinamgoja Sudi kwake,salamu ni Ashua mkewe aliye ndani ya jela.

Majoka anamshauri Sudi anawe mikono iwapo anataka kula na watu wazima.Kunawa mikono ni kukubali kuchonga kinyago ndiposa Ashua mkewe aachiliwe.

Chopi anamwambia Sudi iwapo shamba limemshinda kulima aseme.Shamba anarejelea Ashua kuwa iwapo Ashua amemshinda kutunza, aseme atunziwena Majoka.

Siafu huwa wengi na si rahisi kuwamaliza.Siafu ni wanasagamoyo ambao ni wengi kuliko Majoka na si rahisi kuwashnda.Hatimaye raia wanamshinda Majoka. (uk52)

Tunu anasema kuwa moto umewaka na utateketea wasipouzima.Moto ni harakati za mapinduzi Sagamoyo .Kuteketea nice kumng`oa Majoka mamlakani.

Hashima anamwonya Tunu asijipeleke kwenye pango la joka.Pango la joka anarejelea majoka na watu wake ambao ni kati na wauaji.

Majoka anadai lazima mtu mmoja atolewe kafara ili watu wajue kuwa kuna usalama Sagamoyo.Chatu anamrejelea Sudi au Tunu ambao ni tishio kwa uongozi wake na kuwatoa kafara ni kuua mmoja wao ili kukomesha maandamano.

Majoka anaposema yupo kwenye chombo cha safari ya jongomeo anamaanisha kuwa mwisho wake uko karibu kuondolewa mamlakani.

Kinyago cha mke mrembo shujaa anachochonga Sudi kinaashiria Tunu ambaye ni shujaa wa kweli Sagamoyo

Husda anafananishwa na chui anayeishi ndani ya ngozi ya kondoo kuashiria kuwa yeye ni mnafiki. Hana mapenzi ya kweli kwa Majoka ila aliolewa naye kwa sababu ya mali.

Jazanda ya marubani ambao hawaendesha vyombo vyao vizuri ni viongozi ambao hawaingozi kwa haki. wamejawa na ulaghai na tamaa.(uk80)

Babu anamwambia Majoka kuwa hawezi kuelewa mambo kwa vile hajapambua ngozi yake ya zamani.Majoka anapaswa kubadili mienendo yake mbaya.

Chombo anachopanda Majoka kinaenda kinyume badala ya kwenda mbele, Majoka hajafanya maendeleo Sagamoyo kwa sababu ya ufisadi na tamaa.(uk81)

Kisima kuingiwa na paka maji hayanyweki tena.Sagamoyo ni dhiki tele,hakukaliki kwa kuwa na shida nyingi;soko kufungwa, mauaji kutekelezwa na unyakuzi.

SADFA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Majoka akiwa ofisini mwake,Ashua anaingia bila kutarajiwa.

Ashua akiwa na Majoka ofisini,Husda anaingia bila kutarajiwa,Ashua anamaka na kubakia kinywa wazi.

Majoka anaposoma gazeti anaona maoni kuwa Tunu awanie uongozi Sagamoyo,hakutarajia kuyaona maoni hayo gazetini.

Chopi wanapozungumza na MajokaMwango anafika na habari kuwa Majoka ana wageni, Tunu na Sudi ambao hakutarajia.

Majoka anapongojea Husda katika hoteli ya kifahari Sagamoyo, Kenga anafika na habari kuwa mipango haikwenda walivyopanga,kuwa Tunu bado yupo, hakuvunjwa miguu, Majoka hatarajii Tunu kuwa mzima.

Ni sadfa kwa kifo cha Ngao Junior kutokea sawia na kifo cha Ngurumo.

Majoka anazirai siku kabla ya sherehe ya uhuru, anapopata habari kuhusu kifo cha Ngao Junior.

Inasadafu kuwa siku ya sherehe ndio waandamanaji wanakuwa na mkutano katika soko la chapajazi wakati ambapo wanatarajiwa juhudhuria sherehe.

WIMBO KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

WIMBO WA UZALENDO.

Wimbo huu unaimbwa katika kituo cha habari cha wazalendo,ni wimbo unaosifu Sagamoyo na kiongozi wake kuwa;

Sagamoyo ni jimbo tukufu, wanamtukuza Ngao kuwa kiongozi shupavu.

Maudhui katika wimbo huu ni kinaya kwa vile Majoka sio kiongozi shupavu,uongozi wake una dosari.(uk5)

WIMBO WA HASHIMA.

Anaimba wimbo huu akiwa nyumbani kwake.Wimbo huu unaashiria kuwa mambo hubadilika, kila siku wasema heri yalipita jana.(uk51)

WIMBO WA MAMAPIMA.

Ni wimbo wa kishairi unaorejela Sudi na Tunu.Mamapima anawashauri wajipe raha kwa kujiunga nao katika ulevi.(uk60)

WIMBO WA NGURUMO.

Ngurumo anaimba wimbo kwa mamapima akimrejelea Tunu. Ni wimbo wa kumsuta Tunu kwa kuwa yeye ni mwanamke anapaswa kuolewa.

WIMBO WA UMATI.

Umati unaimba wimbo katika lango la soko la chapakazi.Watu wanaimba kuwa yote yanawezekana bila Majoka.Wimbo huu unasifia juhudi za Tunu kuikomboa Sagamoyo na kuleta uhuru halisi.

WIMBO WA ASHUA.

Ashua anaimba kuwa soko lafunguliwa bila chopi kumaanishwa vikaragosi hawana nguvu dhidhi ya wanamapinduzi.(uk92)

USHAIRI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Majoka anatunia ushairi kupitisha ujumbe wake kuwa Ashua anamuumiza Majoka moyoni kimapenzi.Kuwa anamkondesha na kumkosesha raha kwa kumkataa. Ashua kumkimbia alimwachia aibu Majoka na penzi lake kwa Ashua linamsongoa.(uk76)

Ushairi wa babu,anamshauri Majoka abadili mienendo yake,asikie vilio vya wanasagamoyo ,aone maovu anayoyatenda, ahisi dhiki zinazowakumba wanasagamoyo.

Anamshauri kuwa maisha ni njia mbili:mema na maovu na kuwa maovu yana mwisho.

NDOTO KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Tunu anaotandoto kuwa anafukuzwa na mzee Marara akitaka mkufu wake wa dhababu.

Mzee marara kumfukuza Tunu ni ishara kumkomesha asiwe kiongozi Sagamoyo (kumnyanganya mkufu), mkufu wa dhahabu ni ishara ya uongozi.(uk53)

Majoka anasema na babu katika ndoto.Babu anamshauri Majoka abadili mienendo yake na asikie vilio vya wanasagamoyo.

Babu anamwonya Majoka dhidi ya kuishi kwa kutojali na kumwambia Majoka atende mema.

TAHARUKI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Kombe na Boza wanaagizwa wachonge vinyago, je wanavichonga?

Majoka anampenda sana Ashua, anampata?kama hakumpata, alifanya nini?

Ashua anaomba talaka yake akiwa jela,je anapewa?

Kuna wafungwa ambao wamefungiwa, walifanya kisa gani?je wanaachiliwa? iwapo hawakuachiliwa, hatima yao ilikuwa ipi?

Wageni wanatarajiwa Sagamoyo siku ya uhuru.Je wanafika?

Mpango wa Majoka kumsafirisha Chopi kwa kushindwa kumvunja Tunu mguu, je anasafirishwa? iwapo anasafirishwa, anachukuliwa wapi na kufanyiwa nini?

Anwani ya tamthilia, kigogo ni nani? anafanya nini na wapi?

Kuna taharuki kuhusu kifo cha Ngao Junior.Ni kipi kinasababisha kifo chake?Majoka na Husda wanafanya nini?ni nani atakuwa mrithi wa Majojka katika siasa?

Hoteli la kifahari Majoka analotaka kulijenga baada ya kufunga soko, je anafaulu kulijenga?

Majoka anaagiza Ngurumo azikwe kabla ya jua kutua, je anazikwa?watu wanasema nini kuhusu kifo chake.

MBINU REJESHI/KISENGERE NYUMA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Majoka anakumbuka hadithi kuwa binadamu siku zote humwauni kuku na kumhini kunguru.(uk22)

Majoka anarejelea siku Ashua alipokataa pete yake ya uchumba kuwa hiyo ndiyo siku aliyojikosea heshima na sasa hangekuwa ombaomba.

Majoka anarejelea kisa cha kifo cha Jabali na wafuasi wake, jinsi walivyopanga njama na kumwangamiza.

Ashua anakumbuka mengi Sudi aliyomwahidi siku zao za kwanza za mapenzi.

Tukio la Mzee Marara kumfukuza Tunu ndotoni ni la zamani, la utotoni.

Hashima anakumbuka jinsi alivyoathirika na marehemu mume wake, Marara na watu wake waliwatendea ukatili.

Sudi akiwa kwa mamapima anakumbuka mashujaa waliofungwa wakati wa ukoloni. Mashujaa hao waliangaisha wakoloni na hata wengine wakaenda jongomeo. (uk59).

KIANGAZAMBELE KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Maoni gazetini kuwa Tunu awanie uongozi Sagamoyo,baadaye Tunu anakuwa kiongozi baada ya kumpindua Majoka.

Majoka anahofia kuwa maandamano yatatia doa sherehe za uhuru, siku ya sherehe, watu hawahudhurii.

Majoka anahofia kuwa waandamanaji watafika ofisini wammalize.Mwishowe wanammaliza wanapomtoa mamlakani.

TAMATHALI ZA USEMI.

METHALI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Fuata nyuki ule asali (ukitaka kula asali kaa na nyuki) (uk7).

Methali hii imetumika kuonyesha kuwa ukitaka kupata kitu, kaa na walionacho.

Asiya na Ngurumo walimwandama Bi. Husda hadi wakapata kandarasi ya kuoka keki.

Chelewa chelewa utapata mwana si wako.

Boza, Kombe na, Sudi wasichelewe kuchonga vinyago ili wafaidi, na majina yao yajulikane nje.(uk9)

Mbio za sakafuni, huishia ukingoni.

Kenga anatumia methali hii kurejelea kuwa harakati za Tunu kuleta mabadiliko Sagamoyo hayatafanikiwa.Kauli hii ni kinaya,(uk12).

Udongo haubishani na mfinyanzi.

Wenye nguvu hawabishani na wanyonge.Boza anatumua methali hii kumwonya Sudi asibishane na Majoka anapodai kuwa keki wanayoletewa ni makombo.(uk13)

Aketiye na cha upele,haishi kujikuna.

Sudi anatumia methali hii kurejelea Kombe anapomuunga mkono na kusema mambo yamekwenda kombo Sagamoyo.(uk15)

Simba hageuki paka kwa kukatwa makucha.

Kuwa Majoka alikosa fursa ya kumwoa Ashua haimanishi hana uwezo wa kumfanyia lolote.(uk21)

Kuvuja kwa pakacha ni nafuu kwa mchukuzi.

Kuvunjika kwandoa ya Ashua au Ashua kutalikiwa itakuwa heri kwa Majoka ili ampate Ashua

Heri kufuga mbuzi,binadamu wana maudhi.

Majoka anatumia methali hii Ashua anapokataa ombi lake.(uk26)

Kila mwamba ngoma, ngozi huivuta kwake.

Kenga anarejelea wafadhili wa gazeti kuwa walimtetea Tunu na habari kumhusu zimetiwa chuvi.Waandishi wa gazeti ni wafadhili wa Tunu.(uk33)

Dalili ya mvua ni mawingu.

Tunu huenda akaongoza Sagamoyo.(uk34)

Ukitaka kuwafurusha ndege, kata mti.

Kenga anamrejelea Jabali, kuwa ukitaka kuwaangamiza maadui ua kiongozi wao.Jabali alikufa na wafuasi wake kumfuata ahera.(uk35)

Udongo uwahi ungali mbichi.

Wangemkomesha Tunu kabla ya kupata umaarufu.

Asante ya punda ni mateke.

Majoka anamrejelea Tunu kwa kumpinga baada ya kugharamia masomo yake baada ya kifo cha babake.

Maji ukiyavulia nguo yakoge.

Majoka amekubali kuhukumiwa na kujibu mashtaka kwa kutowajibika kwake na kusaliti nchi yake.(uk79)

MASWALI BALAGHA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Hiyo rununu hitulii mfukoni, yakuuma?(uk1)

Kwani umeota pua ya pili? (uk1)

Kwani u mjamzito? (uk1)

Kwa nini washerehekee mwezi mzima?(uk5)

Eeh!viini ni nini? (uk16)

Hujayaacha hayo?

Siwezi nini? (uk21)

umenizidi kwa nini?

*mwanafunzi atoe mifano zaidi.

KUCHANGANYA NDIMI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

look at the bigger future man (uk18)

Its for our good

what? (uk35)

But one stone is enough (uk36)

Live coverage.(uk38)

Over my dead body(uk45)

Ni afadjali iwe one touch (uk68)

Chopi,time is money.Humjui Asiya (uk71)

*mifano zaidi.

NIDAA KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Linanuka fee! (uk1)

Enhe! (uk19)

Kisa na maana ni wewe! (uk26)

Chunga ulimi wako! (uk27)

Na wewe! (uk27)

TAKIRIRI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Siwezi suwezi, mimi siwezi.

Kila kitu ni Tunu,Tunu,Tunu,Tunu (uk48)

TASHBIHI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO

Ashua angeishi kama malkia.

Husda hataki jua lifanye ngozi yake ngumu kama ya mamba (uk67)

Pengime Tunu atambae kama nyoka. (uk69)

Siku hizi wake hawashikiki, ni kama masikio ya syngura. (uk76)

Kuishi kulivyo ni kama mshumaa. (uk80)


NEXT: MBINU ANAZOTUMIA MAJOKA KUONGOZA SAGAMOYO NA MATAKWA YA WANASAGAMOYO KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO


PREVIOUS: MAUDHUI KATIKA TAMTHILIA YA KIGOGO


dhamira ya mwandishi katika kigogokigogo maudhuikigogo noteskigogo riwayakigogo setbook video downloadkigogo summarykigogo summary noteskigogo tamthiliakigogo tamthilia pdfkigogo videomaswali ya kigogomaswali ya tamthilia ya kigogomaudhui katika kigogo pdfmaudhui ya uzalendo katika kigogomwongozo wa kigogotamthilia ya kigogo videouchambuzi wa riwaya ya kigogowahusika wa tamthilia ya kigogo
Comments (1)
Add Comment